MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal ametoa changamoto kwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuhakikisha inaongeza wigo wa vyuo vikuu vya sayansi nchini.
Pia amesisitiza kuwa Tanzania inaweza kuondokana na tatizo la umasikini iwapo Watanzania watashirikishwa katika taratibu za utafiti na matumizi ya tafiti hizo katika mazingira yao ya kila siku.
Akifungua Maonesho ya Saba ya Elimu ya Juu yaliyoandaliwa na TCU, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Taasisi za Elimu ya Juu nchini, Dk. Bilal alisema pamoja na Tanzania kupiga hatua katika eneo la vyuo vikuu, bado kuna haja ya kuwapo kwa vyuo vingi zaidi hasa vya sayansi na teknolojia.
Alisema ili nchi yoyote ipate maendeleo ya haraka haina budi kuwekeza katika elimu ya juu ili kuongeza idadi ya wasomi na kuhamasisha elimu ya sayansi na teknolojia ambapo pia alishauri utafiti unaofanywa na taasisi hizo usiegemee katika kubaini matatizo, bali na suluhisho la matatizo hayo.
“Ndio maana nashauri TCU iangalie uwezekano wa kuongeza vyuo vingi vya sayansi, hata Serikali imeliona hili na imekuwa ikiwekeza zaidi katika elimu ya sayansi kwa ushirikiano na sekta binafsi,” alisema.
Pamoja na hayo, alisisitiza kuwa taasisi za elimu ya juu katika utafiti wao mbalimbali, hazina budi kuhakikisha zinajikita zaidi katika utafiti wa kisayansi na teknolojia ili matunda ya utafiti huo yatumike katika uzalishaji wa rasilimali za Tanzania badala ya sasa ambapo uzalishaji wa rasilimali hizo unafanywa zaidi na wageni.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema elimu ya juu kwa sasa imepanuka ambapo kuna vyuo 43 tofauti na mwaka 1961 kulipokuwa na chuo kimoja na wanafunzi 13 pekee na kuitaka TCU kuongeza wigo wa vyuo hivyo hasa upande wa sayansi.
Aidha, alizungumzia mfumo wa ada za vyuo vya elimu ya juu alisisitiza kuwa Serikali imeshapitisha maamuzi ya kupiga marufuku vyuo vyote nchini kutoza ada kwa dola isipokuwa kwa wanafunzi wa nje ya nchi pekee.
CHANZO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni