.........BLOG HII BADO IPO KWENYE MATENGENEZO......

Alhamisi, 19 Aprili 2012

Dk. Magufuli augua ghafla, alazwa Dodoma

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa mjini hapa.

Taarifa za kuugua kwa Waziri huyo zilitangazwa jana bungeni na Naibu Spika, Job Ndugai, wakati akiahirisha kikao cha Bunge mchana.

Ndugai alisema awali Magufuli alipelekwa hospitalini hapo akisumbuliwa na shinikizo la damu.

“Baada ya kufika hospitalini na kupatiwa matibabu alibainika kusumbuliwa na kichomi upande wa kushoto… bado amelazwa hospitalini na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikwenda kumwangalia,” alisema.

Pia Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), amenusurika kifo baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, kupata ajali Morogoro. Kwa mujibu wa Ndugai, ajali hiyo ilitokea jana saa 12.15 asubuhi baada ya gari lake kugongwa na lori na kupinduka.

“Gari lote limeharibika, lakini tunashukuru Mungu Mheshimiwa Mbunge na dereva wake wako salama ingawa wamepata majeraha kadhaa na wanaelekea Dar es Salaam kuangalia afya zao,” alisema.

Gari la Mbunge huyo namba T 982 BKQ aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na Hussein Ally (30) mkazi wa Temeke Dar es Salaam, lilipinduka katika kijiji cha Tabu Hoteli, wilayani Gairo, Morogoro kwenye barabara kuu ya Dodoma-Morogoro.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Rugila, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

“Tumepata taarifa ya ajali ya Mbunge Mtemvu…gari limepinduka miguu juu na uchunguzi wa awali umebaini kuwa eneo hilo lilikuwa na utelezi baada ya kunyesha mvua …dereva alishika breki na likageuka lilikotoka , likaparamia nyumba na kupinduka, gari limeharibika vibaya,“ alisema Kaimu Kamanda huyo.

“Nimeambiwa Mbunge ameumia kidogo na dereva wake amepata majeraha madogo begani …waliletwa katika Hospitali ya Mkoa kwa matibabu zaidi na hali zao si mbaya,” aliongeza Kaimu Kamanda.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Marco Nkya, alithibitisha kupokea majeruhi wawili akiwamo Mbunge huyo.

“Ni kweli amefika hapa na dereva wake, wamepokewa Mapokezi (OPD) na kupatiwa matibabu ya majeraha madogo waliyopata...Mbunge alichubuka kiganjani na mkononi, dereva amepata michubuko begani,” alisema Dk. Nkya.

“Hawakuumia kwa kiwango kikubwa cha kufanya walazwe au kutakiwa wapelekwe Muhimbili, tumewatibu hapa OPD, tumezungumza nao akiwamo RAS wa Morogoro, wametuaga na kuendelea na safari yao ya Dar es Salaam,” aliongeza Dk. Nkya. Imeandikwa na Shadrack Sagati, Dodoma na John Nditi, Morogoro
CHANZO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni