FUNDI seremala, Charles Agustino (25) amekamatwa ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala na askari Polisi akiwa anataka kuingiza bangi kwa mahabusu.
Charles maarufu kama Clay, alikamatwa mahakamani hapo akiwa na bangi puli 5 na sigara pakiti saba ambazo zilikuwa zimefungwa katika muonekano wa puli za bangi zikiwa tayari kuingizwa kwa mahabusu hao.
Kwa mujibu wa askari aliyemkamata, Koplo Jonas, awali kijana huyo alifika kwao na kuwaomba kwenda kuzungumza na ndugu yake ambaye alikuwa mahabusu na walipomwambia asubiri, ndipo walimuona kijana huyo akizungumza na nduguye kwa ishara na walipomkagua ndipo wakamkuta na vitu hivyo.
Mtuhumiwa huyo alipelekwa Kituo cha Polisi cha Msimbazi kwa ajili ya kufunguliwa jalada juu ya kosa hilo.
Katika hatua nyingine, wafanyabiashara wawili wamefikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na shitaka la wizi wa pikipiki. Waliosomewa shitaka mbele ya hakimu ni Abdallah Kinyogoli (40) na Ally Kasembo (40).
Wakili wa Serikali Aidah Kisumo alidai Aprili 10, mwaka huu saa nane mchana katika Kituo cha Polisi cha Stakishari, washitakiwa waliiba pikipiki yenye namba za usajili T167 BXH, rangi nyeusi yenye thamani ya Sh milioni 1.7, mali ya Ally Mangole.
Walikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kukosa wadhamini, kesi hiyo itatajwa tena Mei 3 mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni