.........BLOG HII BADO IPO KWENYE MATENGENEZO......

Alhamisi, 19 Aprili 2012

Kikwete asifu msuguano wa Bunge, Serikali

MSUGUANO kati ya Bunge na vyombo vya habari kwa upande mmoja na Serikali kwa upande wa pili, umetajwa kuwa moja ya vichocheo vilivyosababisha Serikali ya Tanzania kuendesha shughuli zake kwa uwazi zaidi kwa maslahi ya wananchi.

Rais Jakaya Kikwete alisema hayo juzi alipokuwa akielezea namna Serikali inavyotekeleza shughuli zake kwa uwazi huku akitaja ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuwa chanzo kizuri cha habari na midahalo katika vyombo vya habari na Bunge.

Akizungumza katika mkutano wa Mpango wa Ubia wa Uwazi Serikalini (OGP) jijini hapa, Rais Kikwete alisema juhudi za kuendesha Serikali kwa uwazi zimekuwa sehemu ya mkakati wa maendeleo ya nchi.

Mpango huo ulioasisiwa na Rais wa Marekani, Barack Obama na wa Brazil, Dilma Varna Rousseff, umelenga kuongeza uwazi na uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi na kuimarisha demokrasia kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya watu, kupambana na rushwa na kuongeza ufanisi.

"Moja ya maeneo tunayofanya vizuri (katika uwazi serikalini) ingawa tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi ni Bunge...hasa wajibu wake katika kusimamia Serikali, bila ukiritimba wala kuingiliwa.

"Vikao vya Bunge vinarushwa moja kwa moja na televisheni na Watanzania wanapata fursa ya kuona wawakilishi wao wakiuliza maswali na kudai majibu kutoka serikalini. Ikibidi Bunge hutengeneza Kamati Teule, kuchunguza jambo wanalolitaka katika uendeshaji wa Serikali," alisema Rais Kikwete.

Alisema hata bajeti ya Serikali na utendaji wa wizara, vinaangaliwa kwa karibu na kamati za Bunge za kisekta na Bunge lenyewe na kuongeza kuwa hata umma wa Watanzania una fursa ya kushuhudia midahalo hiyo ndani ya Bunge na wakati mwingine katika Kamati.

Uhuru wa habari "Sijisifii, lakini naweza kusema kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo wanahabari wamehakikishiwa uhuru wao wa kutoa na kupata habari kiasi cha baadhi kusema kuwa vyombo vya habari vina huru mkubwa uliopitiliza," alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa ushahidi wa hilo ni wingi wa magazeti na majarida ya kila siku, wiki na mwezi.

Aliongeza kuwa kama ilivyo katika magazeti, ndivyo ilivyo katika vituo vya televisheni na redio na kwamba pamoja na wingi huo, Serikali haiingilii utendaji wa vyombo vya habari vikiwamo inavyovimiliki.

"Kuna wakati hata vyombo vya habari vya Serikali vinakuwa vikali dhidi ya Serikali lakini hatulalamiki wala kuviingilia, kwa kuwa vinatekeleza wajibu wao na vinapaswa kuutekeleza vizuri," alisema Rais Kikwete.

Ripoti ya CAG Alisifu ripoti ya CAG kwa kusaidia Watanzania kujua namna fedha zao zinavyotumika serikalini. "Ripoti hii huwekwa wazi kwa kila mtu kuiona na ni chanzo cha habari cha mijadala ya moto na ya wazi ndani ya Bunge.

Ni chanzo cha mjadala mzito katika vyombo vya habari na mitandao ya jamii," alisema. Aliongeza kuwa anafurahi kuona Sheria ya Habari inafanyiwa marekebisho ili kuwapo urahisi zaidi wa kupata habari kutoka serikalini na kuahidi kuhakikisha sheria hiyo inaendana na kanuni za OGP na kuwa na hadhi ya kimataifa.

Katiba mpya Mbali na uhuru wa habari, Rais Kikwete pia alisema yeye na Serikali wanaamini katika kuhusisha wananchi kwenye mambo muhimu yenye maslahi kwao na kwa nchi yao, ameruhusu wananchi watoe mawazo yao katika mchakato wa kupata Katiba mpya ambao alishatangaza kuwa utaanza Mei Mosi.

"Mwaka jana nilitangaza kuwa tutaanza mchakato wa kupata Katiba mpya na nikaweka wazi umuhimu wa wananchi kushiriki moja kwa moja mchakato wa kuipata," alisema.

Alisema muda si mrefu mchakato utaanza kwa kuwa Tume ya Katiba imetangazwa na itazunguka nchi nzima kwa miezi 18 kusikiliza mawazo ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka.

Alifafanua kuwa kwa kutumia mawazo hayo, Tume hiyo itatengeneza rasimu ya Katiba ambayo itajadiliwa na Bunge la Katiba na baadaye itaamuliwa na wananchi wenyewe kupitia kura ya maoni.

"Ni mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, kuanzisha mchakato kama huu, tulikuwa na uwezo wa kuibadili bungeni, kwa kuwa Katiba iliyopo inaruhusu, lakini nilidhani kwa maslahi ya wananchi, tuhusishe wananchi wote.

"Nina hakika tumefuata njia sahihi ya kufikia mafanikio sahihi ya kuboresha utendaji wa uwazi kwa ajili ya kuimarisha Serikali inayojali na kuwajibika kwa wananchi," alisema Rais Kikwete.

Mapambano ya rushwa Kuhusu rushwa alisema Serikali imeboresha sheria ya mapambano dhidi ya rushwa na kuiongezea nguvu na kuiimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

"Matokeo ya sheria hii leo kuna mashitaka mengi ya rushwa mahakamani kuliko wakati wowote katika historia ya nchi, ambayo yanahusu pia viongozi wakubwa wa Serikali wakiwamo mawaziri," alisema.

Aliahidi kuboresha uendeshaji wa Serikali kwa uwazi zaidi ikiwamo kuanzisha Serikali kwa njia ya mtandao (e-government), katika utoaji wa huduma za Serikali. Katika utekelezaji wa hilo, alisema Serikali inafanya uwekezaji mkubwa katika mkongo wa Taifa utakaounganisha ofisi zote za Serikali, ili iwe wazi zaidi kwa wananchi na waifikie kwa urahisi zaidi.

Maliasili isiwe laana Kuhusu uwekezaji katika maliasili, Rais Kikwete alisema miaka mitatu iliyopita Tanzania ilijiunga na Mkakati wa Kimataifa wa Uwazi katika Ugwaduzi (EITI) ili kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika uwekezaji na uvunaji wa maliasili nchini.

"Tunataka mambo yawe wazi zaidi kuanzia wakati wa kutoa leseni mpaka wa uvunaji wa maliasili na uuzaji ili Watanzania wafurahie maliasili zao badala ya kugeuka laana," alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa mifumo ya kuhakikisha hilo, imo katika hatua za awali lakini ina manufaa kwa siku za baadaye.

Mbali na mikakati hiyo ya ndani ya kuendesha Serikali kwa uwazi, Rais Kikwete alisema Tanzania pia ni mjumbe wa Mkakati wa Pamoja wa Umoja wa Afrika wa Kujitathimini (APRM) na kuongeza kuwa miezi miwili iliyopita, Kamati Huru ya Umoja wa Afrika (AU) ya APRM, ilimaliza kufanya tathimini yake na ripoti yake inasubiriwa kwa hamu.

Clinton na Rousseff Awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton aliyemwakilisha Rais Obama, alisema wakati wanabuni OGP, Obama alisema lengo lilikuwa kuboresha uwazi serikalini, kupambana na rushwa na kuhusisha wananchi katika uamuzi wa umma.

Rais Rousseff alisema katika hali yao ya kujiandaa kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia, wameweka uwazi katika ujenzi wa miundombinu na kila mwananchi anaweza kuhoji utekelezaji wa miradi na kufuatilia hatua kwa hatua na ikichelewa, Serikali inawajibika.
CHANZO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni