MKAZI wa Mabibo, Mariam Ally (28) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive akikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kuuza bia zilizokwisha muda wake wa matumizi.
Mariam alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shitaka linalomkabili mbele ya Hakimu
William Mutaki.
Katika shitaka la kwanza, Mwendesha Mashitaka John Kijumbe alidai kuwa Aprili 12, mwaka
huu saa 7 mchana katika eneo la Mabibo katika baa ya Chiluba Park, mshitakiwa alikamatwa na Ofisa Afya Adelaida Morio akiwa anauza bia chupa 35 aina ya miller zenye ujazo wa milimita 330 kila moja ambazo zimekwisha muda wake wa matumizi tangu Februari 2, mwaka huu, wakati akijua hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Kijumbe alidai siku hiyo hiyo, mshitakiwa alikaidi ilani aliyopewa na Ofisa Usafi wa Manispaa ya Kinondoni, ikiwa ni pamoja na kudumisha usafi wa ndani na nje ya jengo hilo.
Hata hivyo, mshitakiwa yupo nje baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na mdhamini na kusaini hati ya dhamana ya Sh 100,000. Mahakama ilitoa amri ya kufungwa kwa baa hiyo na kukamatwa kwa mmiliki wake. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe Aprili 20, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Hassani Kadebele (33) amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shitaka la kujifanya askari wa Jiji maarufu kama Mubamba.
Mwendesha Mashitaka John Kijumbe alidai mbele ya Hakimu William Mutaki kuwa, Aprili 13 mwaka huu, saa moja asubuhi katika mtaa wa Lumumba, mshitakiwa alikamatwa na askari wa Jiji, Magnus Lupindo akijifanya askari wa Jiji na kufanya kazi kama polisi wa Jiji.
Mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo na kurudishwa rumande kwa kukosa wadhamini, kesi hiyo itatajwa tena Aprili 30, mwaka huu.
CHANZO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni