Jumamosi, 21 Aprili 2012
Wabunge wa CCM watishwa
Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa wabunge wa Chama cha Mapinduzi, wameitwa na kutishwa kuchukuliwa hatua ikiwa watasaini azimio hilo.
Mmoja wa wabunge wa CCM aliyekiri kuitwa ni Deo Filikunjombe (Ludewa) ambaye alisema alilazimika kusaini kabla ya kuitikia wito huo.
Filikunjombe, alikiri kuitwa na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na kumtaka kutosaini azimio hilo, lakini akamwambia alikwishasaini na alifanya hivyo kwa niaba ya wananchi wa Ludewa ambao wamechukizwa na ubadhirifu mkubwa uliofanywa na watendaji hao wa serikali.
Kuhusu wabunge wa CCM kutosaini azimo hilo, Filikunjombe alisema kanuni haikusema wabunge wote, kwani inafahamika wengine wanarudi nyuma alisema.
Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde alisema suala la hoja ya kikanuni ina lengo la kuchelewesha mchakato wa kuwaondoa wanaolalamikiwa na kuahidi kuwaondoa hata kama Bunge litawakingia kifua.
Alisema kama mawaziri wanaolalamikiwa wataendelea kubakia katika nafasi zao ni bora wabunge wa CCM wakaondoka na kuwaachia wao majukumu yote.
Alipoulizwa kama msimamo wake hauwezi kuwakera viongozi wake na kuamua kumchukulia hatua ikiwa ni pamoja na kumuondoa katika chama, Lusinde alisema kuwa hilo halihofii kwa kuwa hana hati miliki ya ubunge wa Mtera na zaidi ataendelea kubakia Mtanzania anayepigania maslahi ya nchi yake.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema katika mapendekezo yaliyoafikiwa juzi hakuna azimio katika kamati yoyote lililotaka waziri aondolewe na kusema kuwa alichokuwa akikifanya Zitto ni usanii.
“Katika taarifa yake ile alipaswa aseme Bunge limependekeza mtu fulani awajibishwe, hivyo alitakiwa kuleta nyongeza katika taarifa yake. Hakuna aliyeleta. Ile ni burudani tu,” alisema na kuongeza kuwa hoja hiyo haina mashiko.
Alihoji kuwa iwapo Pinda alishindwa kumuondoa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, atawezaje kumuondoa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.
Alisema kuwa ili hoja hiyo ifanikiwe ni lazima Spika aridhike kwamba ilifuata taratibu na ina sifa hata ikisainiwa na wabunge 200 kama haina sifa haiwezi kupita.
CHANZO
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni