MATUMIZI ya miwani, hususani kwa vijana mkoani Mbeya, yamekuwa yakiongezeka huku wengi wakiamini kuwa ni urembo au mikogo tu ya vijana, lakini kwa wataalamu wa afya, hilo ni tatizo la uoni hafifu linalokua kwa kasi hivi sasa nchini.
Katika moja ya shule za sekondari jijini Mbeya, Raia Mwema ilielezwa kuwa wanafunzi 20 kati ya 200 waliojiunga kidato cha kwanza mwaka huu, wanatumia miwani kutokana na tatizo la uoni hafifu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Luis Chomboko, analibainisha tatizo hilo akisema Mkoa huo kwa sasa unakabiliwa ongezeko la tatizo hilo miongoni mwa wakazi wake, lakini wakati huo huo akionyesha hofu yake katika kukabiliana nalo kutokana na kudorora kwa huduma ya afya ya macho mkoani humo kunakosababishwa na uhaba mkubwa wa wataalamu.
Miongoni mwa matatizo yanayoikabili huduma hiyo ni pamoja na upungufu mkubwa wa wataalamu, upungufu wa vifaa, mwamko na uelewa mdogo wa jamii kuhusu matatizo ya macho na tiba zilizopo.
Dk. Chomboko anasema moja ya mikakati ya kukabiliana na tatizo la macho ni wananchi wenyewe kuwahi kupata matibabu ili kuzuia upofu tangu utotoni hadi uzeeni.
“Tatizo la ugonjwa wa macho linanzia kwa mgonjwa mwenyewe, mtu haumwi, mgonjwa hajisikii kuumwa hivyo hukaa tu nyumbani, tunalazimika kuwafuata wananchi kuwaelimisha ili wapimwe,” anasema Dk Chomboko.
Ukiweka kando tatizo hilo la wananchi kutohiari kwenda kupima afya zao za macho, kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu huyo, Mkoa wa Mbeya unakabiliwa na tatizo sugu la uhaba wa wataalamu wa macho.
Hospitali ya Mkoa, mathalani, haina daktari bingwa, wasaidizi na wauguzi hata mmoja, huduma zake zinamtegemea zaidi mtaalamu wa kuangalia afya ya jicho na kutoa miwani.
Katibu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dories Nzigirwa anabainisha hali hiyo akisema:
“Hospitali imeomba msaada kupeleka watumishi kusoma, kitengo hakina daktari na wauguzi wa macho, tulionao hapa ni wataalamu wa kuangalia afya ya jicho na kutoa miwani tu.”
Kuongezeka kwa tatizo la afya ya macho mkoani Mbeya kumeibuliwa kupitia utafiti uliofanyika hivi karibuni katika Wilaya ya Kyela mkoani hapa, ilipobainika kwamba asilimia sita ya watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea wana matatizo ya kutokuona na kati ya hao, asilimia 70 inachangiwa na mtoto wa jicho, asilimia nyingine 77 za wenye uoni hafifu walio nje ya umri huo inachangiwa pia na mtoto wa jicho.
CHANZO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni