.........BLOG HII BADO IPO KWENYE MATENGENEZO......

Jumanne, 24 Aprili 2012

TAARIFA YA CHAMA CHA WAFANYAKAZI WA SEKTA YA HUDUMA ZA MTANDAO WA MAWASILIANO TANZANIA KWA VYOMBO VYA HABARI


Katibu Mkuu wa TEWUTA Junus Ndaro akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari Maelezo leo jijini Dar es salaam juu ya matatizo yaliyopo katika makampuni ya Simu n akuhusu punguzp la tozo inayolipwa kwa Tume ya Mawasiliano TCRA katika picha kushoto ni Ahmed Kaumo mjumbe wa kamati ya utendaji ya TEWUTA.


UTANGULIZI

Tanzania Communication Regulatory Authority (TCRA) imeundwa chini ya Sheria Na. 12 ya Mwaka 2003, ikiwa na majukumu ya Utoaji leseni, Usimamizi na Udhibiti wa Taasisi zote za Mawasiliano ya Simu, Posta, Radio na kadhalika.
Katika kutekeleza moja ya majukumu yake TCRA inawajibika kutekeleza yafuatayo:-
-Kusimamia ushindani wa kibiashara kwa lengo la kukuza uchumi.
-Kusimamia huduma kwa wateja.
-Kusimamia huduma bora.
-Kusimamia bei za huduma (tariffs rate).

MAKAMPUNI YA SIMU YANCHUNGUZWE KATIKA ULIPAJI KODI.
Awali ya yote tunakiri kuutambua vema uongozi wa TCRA na majukumu yake, ambayo kimsingi uongozi huo unawajibika kuyasimamia vema majukumu hayo kwa faida ya Watanzania wote, chombo hiki kilipoundwa Watanzania walio wengi walitarajia kuwa kitakuwa na uwezo wa kusimamia bei za Mawasiliano ya Simu, na kuhakikisha Sekta hii ya Mawasiliano ya Simu hapa nchini inastawisha uchumi wa Tanzania.
Ni muda mrefu tumekuwa tukifuatilia kwa ukaribu na kujiuliza ni kweli Makampuni haya ya Simu, hususani ya Kigeni yamekuwa yakilipa Kodi kwa mujibu wa Sheria za hapa Nchini, na je kuna chombo huru ambacho kinatambua idadi ya Simu zilizopigwa ili kiweze kuisaidia TRA kukusanya mapato?, jibu ni hapana.

Chama cha TEWUTA tunawaunga Mkono Waheshimiwa Wabunge walipowasilisha hoja Bungeni kutaka Makampuni haya yalipe Kodi na kuhakikisha yanazingatia Sheria zote hapa nchini.
Iwapo Makampuni ya Simu hapa nchini yataachwa yatoe Taarifa za Makusanyo ya Fedha, na pasipo kuwepo na chombo cha kuhakikisha ukweli wa taarifa hizo, tutambue kuwa nchi itakuwa inapoteza fedha nyingi ambazo zingezalishwa kupitia Mawasiliano ya Simu.

Ulipaji wa Kodi ni muhimu sana kwa Ustawi wa Nchi, tusingependa kuona Makampuni ya Simu yanakwepa ulipaji wa Kodi au kuwa Sehemu ya uzalishaji mdogo wa fedha za Kodi kutoka sekta hii ya Mawasiliano.
Sote tunatambua wazi kwamba, Makampuni haya yamekuwa yakizalisha fedha nyingi, pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wateja, tarajio letu ni kuona yanalipa Kodi kwa uhalisia bila kuwepo kwa uchakachuaji wa aina yoyote.

Tunaitaka TCRA kuisaidia Serikali ili kuhakikisha Makampuni haya yanalipa Kodi halali, ikizingatiwa kwamba hili ni jukumu mojawapo kati ya majukumu kadhaa yanayotakiwa kufanywa na TCRA katika usimamiaji sekta ya mawasiliano hapa nchini, na iwapo TCRA itasimamia vema zoezi hili Makampuni yote yataweza kulipa Kodi na Sekta hii ya Mawasiliano itakuwa ni sehemu yenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi hapa nchini.


TOZO INAYOLIPWA TCRA NA MAKAMPUNI YA SIMU NCHINI IPUNGUZWE.
Watanzania walio wengi walitarajia kuwa baada ya kuundwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano (TCRA) itasimamia na kuhakikisha gharama za huduma za mawasiliano ya Simu zinapungua na kuwa na uwiano sawa kwa tozo la Makampuni yote hapa nchini.
Mamlaka imeshindwa kuwaeleza Wantazania kwa uwazi, na huku ikitambua kuwa moja ya jukumu lake ni kupanga bei elekezi (Harmonize price) kwa Makampuni ya Simu, kitendo ambacho hakijafanyika toka Mamlaka iundwe na kutangazwa kwenye vyombo vya habari.

Ni ukweli kuwa Watanzania wamechoka kutembea na simu zaidi ya moja za Mitandao tofauti, kwa sababu ya kutafuta punguzo kwa Mtandao husika, hii hali tutaendelea nayo hadi lini? Hivi ni kweli hakuna Sheria ambazo zitawalazimisha Wamiliki wa Mitandao kuwa na bei zenye uwiano wa karibu, jibu Sheria zipo. Mbona TCRA imelala na kuona Watanzania wananyonywa hadi Senti yao ya Mwisho, tunapaswa kuwajibika.

Ni lazima mtambue kuwa uudwaji wa Chombo hiki ni kumsaidia mtumiaji (Mteja) asinyonywe na iwapo TCRA inasahau majukumu yake, Watanzania wataendelea kuilalamikia Serikali. Wakati sasa umefika wa kusema hapana, kila chombo kiwajibike na kuhakikisha wanaisaidia Serikali ili kuleta utulivu Nchini.
Rejea historia ya nyuma, Wamiliki wa Mitandao walikuwa na hoja ya msingi ya kwamba gharama za uedeshaji wa shughuli za mawasiliano zilikuwa juu sana kwa sababu Mawasiliano yaliwezeshwa kwa kupitia kwenye Satellite, lakini hivi sasa Serikali imetuletea Mtandao wa Mkongo (FIBRE) ambao gharama zake za uendeshaji ni ndogo sana na unafanya kazi vizuri kwa haraka zaidi.
Hivyo basi uwezekano mkubwa wa kupunguza gharama za mawasiliano hapa nchini upo.TCRA katika kuhakikisha kwamba gharama za mawasiliano zinapungua kwa sasa ni lazima ikubali kupunguza gharama zake.
TCRA inapaswa kufanya kama ifuatavyo:-
TCRA inapaswa kusitisha malipo ya Tozo ya maunganisho (Interconnection rate) yanayolipwa kwa fedha za Kigeni (DOLA) kwa Makampuni ya Simu, pia kiwango kinachotozwa bado ni kikubwa na kinapaswa kuondolewa au kupunguzwa kwani hakina faida kwa mtumiaji.

TCRA inapaswa kuondoa au kupunguza gharama za viwango vya kupiga simu (Tarriff) kwa Makampuni yote ya Simu hapa nchini ili kuwa na gharama elekezi.

TCRA inapaswa kupunguza gharama za malipo (TOZO) ya umiliki wa njia za Mawasiliano (Frequency) inayolipwa kwa fedha za kigeni na kiwango kilichopo ni kikubwa.
TCRA inapaswa kupunguza Malipo (TOZO) inayoyatoza Makampuni ya Simu kama gharama za malipo ghafi kwa mwaka (Loyalty fee), ni ukweli kiwango hiki cha asilimia 0.8 ni kikubwa na kinasababisha watumiaji kuumia.

TCRA inapaswa kupunguza gharama za Malipo ya Mawasiliano Vijijini (Rural areas) ya asilimia 0.4 yanayotozwa Makampuni ya Simu.

TCRA inawajibika kutambua idadi ya Simu zote zinazopigwa kutoka Mtandao Mmoja kwenda Mwingine, hili ni jukumu lao na hatukubaliani na Mawazo ya kutafuta Kampuni nyingine ili kufanya kazi hiyo, hayo ni mawazo ya Kifisadi na hayakubaliki.

Kwa kuwa TCRA inaonyesha dhahiri kujali kukusanya fedha tu, na kuacha majukumu yake ya msingi, tunadhani sasa ni muda muafaka wa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kuandaa Mswada na kuufikisha Bungeni ili Malipo yote yanayolipwa TCRA yakusanywe na TRA, iwapo Mheshimiwa Waziri atatekeleza hili TCRA itakuwa na nidhamu ya kusimamia maslahi ya Nchi.

Iwapo TCRA haitatekeleza haya kamwe Watanzania wasahau kwamba kuna siku moja gharama za Simu zitapungua, Chombo kilichoaminika na Serikali katika kudhibiti bei ndio chanzo kikubwa cha upandaji wa bei za gharama za Simu.
Ni lazima tutambue kuwa Uwepo wa Chombo hiki ni kudhibiti bei kwa watumiaji na kuhakikisha Makapuni yote yanakuwa na bei elekezi zenye uwiano mmoja.
Mwisho, tumechoka kubeba Simu nyingi za kila Mtandao tunaitaka Bodi ya TCRA pamoja na uongozi wa TCRA kukutana ili kujadili Bei na kuhakikisha inawapunguzia watumiaji bei pamoja na Makampuni husika.

Imesithibitishwa
JUNUS P. NDARO
KATIBU MKUU TEWUTA
SIMU: 0732 – 200222
0786 – 200224

Imetolewa na kusoma leo tarehe 24 /04/2012 saa tano asubuhi .
CHANZO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni