HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, imeshauriwa kujenga choo na jukwaa kwa ajili ya ibada za mazishi kwa watu wanaoenda kuzikwa katika eneo la Sabasaba, ambalo wananchi hulipia Sh 300,000 kwa ajili ya maziko ya ndugu zao.
Akizungumza wakati wa mazishi ya mwanajeshi mstaafu, Yohana Mangula yaliyofanyika jana, Mwenyekiti wa Mtaa wa Isanga Kati Kata ya Isanga, Mbengale alisema Halmashauri ya Jiji inatakiwa kujenga choo kwa ajili ya watu kujisitiri wanapokwenda katika maziko pamoja na jukwaa kwa ajili ya kuendesha ibada za mazishi.
“Hapa kuna idadi kubwa ya watu wamekuja, lakini hakuna choo hata kimoja, sasa mtu hapa akitaka kujisaidia aende wapi? Lakini pia lijengwe jukwaa kwa ajili ya ibada na kuihifadhi miili kabla ya maziko wakati mvua inaponyesha badala ya majeneza kunyeshewa tu na mvua, haipendezi kwa kweli,” alisema.
Mbengale alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya imekuwa ikihimiza masuala ya usafi lakini kazi hiyo haitafanikiwa ikiwa mazingira ya maeneo ya mazishi ikiwamo ujenzi wa vyoo halitatiliwa mkazo.
Diwani wa Kata ya Isanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji, Duru Mohamed alisema tayari Kamati yake imeshapanga bajeti na ujenzi wa uzio kuzunguka eneo hilo la mazishi, vyoo pamoja na jukwaa unatarajia kuanza mwakani.
Alisema Kamati yake ililiona suala hilo na kwamba lilikuwepo katika mipango ya halmashauri watafanya utekelezaji wa haraka ili kuimarisha usafiri wa mazingira pamoja kulinda afya za watu wanaofika katika eneo hilo kwa ajili ya shughuli za mazishi.
Kwa upande wake kiongozi wa shughuli za mazishi hayo, Charles Mwakipesile alisema kuwa kilichosemwa na Mwenyekiti huyo ni sawa kwa kuwa watu wanalipia eneo hilo hivyo ni lazima kuwa na mazingira bora yasiyohatarisha afya za wananchi.
CHANZO:Imeandikwa na Merali Chawe, Mbeya; Tarehe: 13th April 2012
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni